Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Serikali Yapinga Ripoti ya Human Rights Watch, Yaitaja Kujaa Upotoshaji

  • 3
Scroll Down To Discover

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kusikitishwa na ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Human Rights Watch (HRW) Septemba 29, 2025, ikisema ripoti hiyo imejaa makosa, upotoshaji na tuhuma za uongo dhidi ya Tanzania, na ilitolewa bila Serikali kupewa nafasi ya kujibu.

Akitoa msimamo wa Serikali Oktoba 2, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema inasikitisha kwamba taasisi yenye heshima ya kimataifa kama HRW inachapisha madai yasiyo na msingi ambayo yana lengo dhahiri la kuchafua sifa ya nchi katika ngazi ya kimataifa.

‎”Madai kwamba mamlaka mbalimbali za Serikali zilipewa fursa ya kujibu tuhuma hizo halina ukweli wowote, kwani hakuna mawasiliano yaliyofanywa kwa barua, simu, wala barua pepe” imeeleza taarifa hiyo.

Serikali imesisitiza kuwa inalinda na kusimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo nchi imeridhia.

Aidha, imeeleza kuwa Sheria mpya ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya 2024 imetoa uwanja sawa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Taarifa hiyo imekanusha hoja zilizotolewa na HRW kuhusu kupungua kwa nafasi ya kiraia na vizuizi kwa vyama vya siasa, ikieleza kuwa madai hayo hayana msingi na ni upotoshaji.

‎Aidha imesema kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha haki za binadamu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 na miaka mingine ijayo, kama ilivyokuwa ikifanya kila wakati.

Serikali imeziomba taasisi na mashirika ya kimataifa kuhakikisha yanapata maoni ya Serikali kabla ya kuchapisha ripoti zinazohusu Tanzania.

“Tunatoa wito kwa mashirika yote na wadau kuwasiliana na mamlaka husika kabla ya kutoa ripoti, ili kuepuka upotoshaji wa taarifa unaoweza kudhoofisha sifa ya nchi kimataifa,” taarifa imesema.

Ripoti ya HRW ya Septemba 29, 2025, ilidai kuwa Serikali ya Tanzania imezidisha ukandamizaji wa kisiasa na kuibua hofu juu ya iwapo Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025, utakuwa huru na wa haki.



Prev Post Air Tanzania yatangaza ajira mpya 173
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook